Nilikufa Kitambo

NILIKUFA KITAMBO

Juu ya kitanda alilala mgonjwa ambaye kwa miezi saba sasa hajapata ashekali. Alizingirwa na walokole wakimuasaa Mterehemezi amwonee kite amwepushe na mauti. Mgonjwa wa jana, leo halikuwa si mgonjwa tena anakaribia kuwa maiti. Tofauti yake na maiti ilikuwa moja tu, uhai. Sura yake iliyokuwa nzuri miaka ayami iliyopita sasa ilikuwa inatisha. Ule weupe ulifukuzwa na weusi. Weusi nao ukakita mzizi na kustakimu katika ngozi ya Haji. Haji wa jana si wa leo. Huyo si yule Haji aliyekuwa na sura ya kuvutia. Sikwambii ni mara ngapi wasichana wamempigania baada ya yeye kuwabari na kusonga baidi nao.

Mgonjwa wetu alilala macho kayakodoa pima. Nywele zimemtoka sasa zimebaki mbili kichwa kizima. Mishipa inaonekana kwa urahisi sana. Kama aliyoyafanya katika siku za uzima wake yalikuwa mazuri au mabaya mimi sijui. Itakuwa vibaya kumuhukumu mimi, pengine nikuhadithie kisa kizima ndipo nawe uwe na uhuru wa kumhukumu au kutomhukumu.

*****

Ile siku ya siku miaka miwili iliyopita ndipo Haji alianza kufuata mkondo mwingine wa maisha. Mkondo ambao ungemuuliza yeye siku hizo angekuambia kuwa ndio mkondo wa kisasa. Usasa ulimponza. Siku yenyewe kama siku zingine ilianza kwa uchangamfu kijijini Banda. Ilikuwa siku ya kawaida kwa viumbe wote isipokuwa Haji. Wazazi wake walikuwa wametangulia kuamka kuelekea kondeni. Huko walifanya kazi siku nzima. Mama mtu kajifunga bwende kiunoni aking’oa magugu na dada mtu kashika kiserema akilima. Na usikibeze kiserema kwani wasemao husema kiserema kimelima kimeshinda jembe nzima.

Kukosekana kwa familia nzima pale nyumbani kulimpa Haji faragha ya aina fulani ambayo alihitaji. Naam, faragha ambayo ilmwezesha Jamila kuja bila kuonekana asubuhi ile. Saa nne kamili ndio muda waliokuwa wameagana, na Haji alizingatia hili la muda sana manake alikuwa na miadi mitatu siku hiyo. Wa kwanza tayari ameshawahi. Jamila msichana aliyeumbwa kaumbika alikuwa na kila sifa ya mwanamke mrembo. Kule kucheka kwake na tabasamu la mnato kuliwatia wengi tumbo joto. Na kila anapotabasamu vidu hutokea kwenye mashavu. Hapo naye urembua macho yake yenye ulaghai wa kimapenzi na kukutazama. Mwanamume yeyote angelambatia. Kifua chake chenye madodo mawili yaliyosimama tisti ndiyo hasa kilichomvutia Haji mpaka akamtongoza. Ongeza na umbo lake na mwendo wake wa kunesa. Nakwambia huyu si wa dunia hii. Ametokea peponi.

Mlango wa nyumba ya Haji ulifunguka polepole, Haji mwenyewe alikuwa kaketi juu ya kitanda. Anangoja, na angojaye hachoki eti. Msichana mrembo aliyevalia buibui jeusi alisimama mbele yake uso kainamisha chini kwa haya. Mikononi na miguuni kachorwa ina.

“Za saa hizi Jamila?” alimsalimu Haji kwa tabasamu. Tabasamu ambalo lilivutia wengi hasaa vigori. Na si tabasamu tu. Haji alikuwa mtanashati kupindukia. Wengi walimtamani hata wake za watu. Sikwambii mke wa Yusuf jirani yao Bi. Shombe.

Kimya kilishamiri baina ya wahusika hawa wawili, Jamila akashindwa kujibu salamu. Salamu kama hizo hazikustahili kujibiwa kulingana na yeye. Hazikuwa na umuhimu wowote. Kilichokuwa na umuhimu wahusika wote wawili walikijua na baaada ya muda walianza kukifanya. Mpororo wa matukio ulianzia, ukafuatana miguno ya sauti ya juu. Miguno iliyodhihirisha raha wanayoipata wahusika hawa wawili. Jamila akajisahau akawa anaguna kwa sauti ya juu iliyomvutia Bi. Shombe ambaye alikuwa anapita karibu na chumba cha Haji. Akasita ghafla na kuanza kudoya, alipendezwa na sarakasi zile. Shauku ya kutaka kuona ikampanda hadi akasogelea karibu na mwanya ambao ulikuwa mlangoni karibu na bawabu za mlango. Hapo aliona wahusika wawili wakiwa uchi miili imeloa majasho.

Kila mmoja wao alionekana kutabasamu. Haukupita muda Jamila na Haji wakawa wanavaa mavazi yao, Jamila yu tayari kuondoka naye Haji ataka kumsindikiza. Bi. Shombe kuona hayo alijibanza karibu na kichaka kilichokuwa karibu akawaona Haji na Jamila wakifuatana kutoka nje huku wana tabasamu. Nyoyo za wote wawili zinaterereka kwa furaha. Kila mmoja ametimiza lengo lake.

“Nifikishe hapa niko sawa Haji. Tutaonana” alisema Jamila kwa furaha.

“Sawa basi mpenzi tutawasiliana” Haji alisema huku akigeuka kurudi nyuma. Hata leo sijapata kujua mbona baada ya watu kufanya mambo fulani huwa hawasemi sana wakiwa njiani. Nadhani huwa wanatafakari mambo waliyofanya. Huo ni mtazamo wangu sijui wako ni upi.

Haji alipofika kwake alimpata Bi. Shombe kajilaza kitandani kifuani amejifunga kanga.

“Unafanya nini hapa Bi. Shombe jamani?” alimuuliza Haji huku akiwa ameachama.

“Nimekuja nami unipe ulivyompa huyo binti. Kumbe wewe fundi na hukuniambia. Mwanzoni nikidhani wewe ni dumaa” Bi. Shombe alisema kwa sauti ya mapenzi.

“Jamani wewe umenizidi umri. Nina miaka ishirini na miwili tu wewe una thelathini na kitu. Tena wewe mke wa mtu na mke wa mtu sumu” alikaidi Haji.

“Wembamba wa reli garimoshi hupita juu. Na hata gari liwe refu vipi nafasi ya dereva ni ileile jamani Haji kipenzi usinikoseshe raha nakutamani mwenzangu” alimrai Bi. Shombe huku akimjongelea Haji.

“Mke wa mtu sumu kaniambia bibi” alimkumbusha.

“Kama ni sumu basi ni sumu tamu” alimjibu Bi. Shombe huku akifungua vifungo vya shati la Haji.

Haukupita muda mwingi kabla ya Haji kujipata kitandani na Bi. Shombe akiiramba ile sumu aliyoonywa na Bibi yake Biti Fatuma. Baada ya kuionja sumu yenyewe alisadiki maneno ya Bi. Shombe kuwa ni sumu tamu. Ama kweli sumu ya neno ni neno.

Baada ya Haji kuonja sumu yenyewe aliona kumbe si sumu isemavyo. Kumbe ni uki mtamu. Naye Bi. Shombe alisadiki kuwa umri ni nambari tu.

“Kwanzia leo mimi nitakuwa nakupa chochote unachohitaji. Wewe ni kusema na mimi ni kukupa tu” alisema Bi. Shombe huku akijipangusa jasho kwa taulo.

“Nitaanza kwa kukununulia simu na kukukodia chumba mjini ambako nitakuwa nakutembelea kila Ijumaa. Nitakuvalisha ung’ae. Mtanashati ulipo hauhitajiki kukaa shamba kama wengine. Wewe umeumbiwa mji” aliendelea kumpa ahadi nyingi Bi. Shombe.

Na zote kapania kutimiza. Na mbona asitimize? Dude liitwalo fedha kwake si kitu. Mwanzo mumewe Yusuf ni wakili ambaye ni maarufu sana. Kipato chake kinaweza lisha familia kadhaa pale Banda. Bi. Shombe mwenyewe naye ni mkulima. Amepanda mimea lukuki ambayo kila siku gari hukujia kwenda kuuzwa mjini. Na pengine sababu hii ya kuwa mkulima ndiyo inayomuweka shamba. Aachie nani shamba lake la ekari mia mbili?

Siku ile ndiyo siku maisha ya Haji yalibadilika. Kukutana na Bi. Shombe siku ile ilikuwa nyota ya jaha. Nyota ambayo ilimtoa Haji kijijini Banda hadi mjini. Huko mjini aliishi jumba la kifahari. Jumba ambalo Bi. Shombe mwenyewe ndiye mmiliki. Na si hili jumba tu. Anamiliki majumba mengi sana na maduka kadhaa ambayo yanauza vifaa vya kielektroniki. Kwake umaskini lilikuwa neno ambalo lilikosa katika kamusi ya taamuli yake. Haji naye akawa na ina kuwa pesa hazitakosa. Wajibu wake ulikuwa mmoja tu. Kumpa raha Bi. Shombe kila Ijumaa. Raha ambayo aliikosa kwa mume wake Yusuf pengine kutokana na shughuli nyingi za mumewe au pengine kwa sababu zingine ambazo Bi. Shombe alizijua mwenyewe.

Haji alipofika mjini ndipo mji ulipomwonyesha mengi ambayo umefumbata. Kwanza mji ulimfunza kuwa hakuna linalokosekana mjini maadamu una pesa. Na pesa ndicho walichokosa watu wengi isipokuwa Haji na wachache wengine. Mji ulimfunza kuwa siku ya Jumamosi ni siku ya kukesha vilabuni na wanawake. Hakuchelea kumpata binti aliyeitwa Muna ambaye raha zote kaumbiwa yeye binti huyu. Muna alimwonyesha vilabu vya nguvu kama wasemavyo wa mji. Ikawa kila Jumamosi ni Haji na Muna, Muna na Haji. Ni mtu na kivuli chake hasaa. Kila hoteli ya thamani waliingia, wakala na kulala. Walipolala hawakulala usiku mzima. Nusu ya usiku walikuwa macho wakifanya hili ama lile. Sana sana lile ambalo dini yao ilikataza isipokuwa kwa watu waliooana tu. Hawa waliingililia anasa na mapenzi ya kiholelaholela wakiwa wachanga. Ikawa Ijumaa ni Bi. Shombe na Jumamosi ni Muna.

Kosa alilofanya Haji ni kuingiliana kimwili na Muna bila kuwa na tahadhari yeyote. Ule urembo wa binti huyu ulimfumba macho Haji asikumbuke dude liitwalo mpira. Halisahau dunia imeharibika na magonjwa yamekuwa mengi sana ulimwenguni. Magonjwa mengine ambayo hayana tiba yapo pia. Viumbe hawa wawili hawakukumbuka chochote isipokuwa raha tu.

Ugonjwa wa kwanza alioanza kuugua Haji ulikuwa ule ugonjwa auguao mwanamume yeyote yule mwenye pesa. Ugonjwa wa kutamani kila kiumbe ambacho ni cha jinsia tofauti naye. Yaani wanawake. Katika kutamani kwake Haji hakuwa na mipaka alitamani mwana na hata mama ya mwana. Ni mara si moja alijipata ana uhusiano na binti na mamake. Mfano bora ni ule wa msichana aliyeitwa Riziki na mamake Tunu. Alivyokutana na Riziki ilikuwa sadfa. Walikutana njiani. Siku moja Riziki akiwa ametoka chuoni akawa amekosa gari la kumfikisha kwao nyumbani. Ambapo ndipo Haji alipoona mtoto wa kike anatembea njiani peke yake mida ile ya usiku. Huruma ukamwingia kama sijaita huruma tamaa. Akambeba Riziki hadi kwao. Hatua chache kabla ya lango la kwa akina Riziki lilibaki gari la Haji katika giza totoro. Akazima taa za mbele na nyuma na kuacha giza litawale. Giza nalo likaja na kuungana nao katika mazungumzo yao.

Mazungumzo yalipofika kilele Riziki akadhani amepata kumbe kapatikana. Alipoagwa na Haji akagitagita. Haji naye kuona mwana anaganzaganza akatafsiri kitendo kile kwa njia yake. Njia ambayo ilijaa uchu tu. Hapo ndipo Riziki na Haji walijipata wamelaza kiti cha gari wanafanya kile ambacho Haji amezoea kufanya naye Riziki ndio mara ya kwanza anakifanya. Walipomaliza Riziki aliomba kuondoka huku Haji akimwaahidi kuwa angekuja kesho kumchukua. Kumchukua ili amwonyeshe dunia. Naye asione dunia vipi na dunia i mikononi mwa Haji. Siku hizi anaruka atakavyo. Asubuhi yuko Marekani saa saba mchana anakula chamcha Uingereza. Jioni anabarizi Afrika Kusini na usiku analala Uarabuni.

Asubuhi saa tatu ilimpata Haji akibisha mlangoni mwa akina Riziki.

“Riziki yupo” alimsaili Tunu mamake Riziki.

“Ametoka kiasi msubiri yuwaja” alimjibu kwa bashasha. Bashasha ile iliashiria mambo mawili. Mosi ni yale mavazi aliyokuwa amevaa Haji. Suti Nyeusi na viatu vyeusi pamoja na koto nyeusi. Na pili ni kupendezwa na kijana wa kiume aliyesimama mbele yake.

Waliosema ngoja ngoja huumiza matumbo hawakukosea. Na baada ya matumbo ya hawa wawili; Tunu na Haji kuumia waliamua kuyapoza. Kwa muda wa saa nzima walikuwa wakitazamana tu hakuna anayesema. Kilichomvuta Tunu hadi alipokuwa Haji naweza kusema kuwa ni aina ya sumaku ivutayo viumbe wala si vyuma.

Riziki alipoingia alimkuta mamake mzazi sakafuni kando yake Haji. Ndio mwanzo wanamaliza shughuli. Na shughuli yenyewe haikuwa ndogo weye ilionekana kubwa. Kama isingekuwa kubwa mbona zulia lilikuwa limejikunja? Kama haikuwa kubwa mbona wahusika hawa wawili walisahau kwenda chumbani? Kama haikuwa kubwa mbona makochi yalikuwa yamepanguliwa?

“Umenisaliti Haji. Moyo wako umejaa uchu tu. Haukutosheka na mimi sasa umeona uzini na mama’ngu mzazi? Wewe si mtu wewe ni shetani toka nje” sauti yenye hasira ilisema.

Haji alitoka huku akimwacha mwana na mamake wakitazamana. Akatia gari moto na kuondoka.

Alipotoka hapo alifululiza hadi kwa Muna ambaye alikuwa amempeza kitambo. Huko nako hakutulia baada ya kuvuta kokeini alianza kufanya yale aliyoyazoea. Almuradi mapenzi kwa Haji yalikuwa kama kunywa maji. Na maji ni uhai kumbuka. Hela zote alizopewa na Bi. Shombe ambaye naweza kusema alikuwa mfadhili wake ziliishia kwa wasichana hadi pale Haji alipoanza kuabudi kitu kingine tofauti na wasichana. Kitu hicho kiliitwa pombe. Alilewa mchana na usiku. Na yote haya kamfunza Muna. Siku hizi hamna klabu hakimjui Haji. Anaweza hata kukopa pombe. Mbona asikopeshwe na yeye ni mteja mkubwa?

Walilewa chakari wakiwa na Muna. Sikwambii ni mara ngapi alilala vilabuni, mitaroni na hata kwenye veranda za majirani wao.

Siku moja walipokuwa njiani wakitoka kunywa shira mbali na mji walipita karibu na kilinge cha wachawi.

“Nitakununulia ndege Muna…..naku..pend…aaaaa” ilisema sauti ya kilevi yake Haji.

“Kina nao hao. Ndegere hebu nenda uangalie” ilisema sauti ya mchawi mmoja maarufu sana. Ilisemekana ana uwezo wa kupaa.

“Mbona mnatusumbua?” aliwauliza Ndegere msaidizi wa mchawi aliyemtuma.

“Nitakunyofoaaaaaaa” alimjibu Haji kwa jeuri.

“Nitakufanya kuku wewe kijana usicheze nami” aliendelea kumtishia Ndegere.

“Waaaapi. Vitisho baridi” alisema Muna kwa beuo.

Kufumba na kufumbua macho Muna alikuwa hayupo. Jogoo mweupe alionekana akitokomea vichakani. Haji kuona hivi alitimka mbio. Pale pakawa hapamuweki tena.

Alipoamka kesho yake alidhani kuwa kaota Muna amefanywa jogoo lakini baadaye alikuja kujua haukuwa utani. Muna hakuonekana tena. Kwa sababu ya mzongo wa mawazo Haji alijipata akinywa pombe ili kusahau. Akawa halali kwake. Akasahau kuwa alikuwa na wajibu wa kutimiza kila Ijumaa kwa mtu ambaye ndiye haswa alikuwa chemchemi ya pesa kwake.

Chemchemi nayo ilitoa maji yakajaa. Pakawa hapana wa kuyachota maji. Aliyestahili kuyachota alikuwa kageuka mlevi siku hizi. Analala vilabuni tu kila uchao. Bi. Shombe alipoona Haji hamtimizii mahitaji yake aliamua kumwacha. Akachukua jumba ambalo alikuwa kampa mwanzoni na kila kitu. Haji alibakia hana chochote. Akashindwa kabisa kuendelea kuishi maisha yake ya awali. Akawa sasa anastakimu katika maganjo tu ambayo hayana hadhi. Watu walipomwona walisema huyu si yule Haji wa jana.

Kama mpanda ngazi hushuka basi Haji hakushuka alianguka hasa. Kuanguka kutoka juu hadi chini. Machangani tifu! Akabaki kiumbe ambacho hakina maana. Kule kukonda ghafla ndiko kulikompa wasiwasi sana yeye na watu wanaomjua. Maradhi yakawa hayamwishi na alipopimwa aliambiwa anaugua kaswende na UKIMWI. Magonjwa mawili tofauti japo asili ni moja. Yote yanatokana na zinaa japo ugonjwa mmoja kati yao hauna dawa. Ugonjwa wa kaswende ulimtafuna sehemu za siri zikawa zinatoka usaha na ugonjwa wa UKIMWI ukamtafuna mwili mpaka akabaki dubwasha la binadamu.

*****

Imepita sasa miezi saba na mgonjwa wetu haoneshi matumaini. Walokole waliomzingira waliamini sasa watampoteza pale walipoona ameanza kufafaruka. Madaktari walikuwa wamekwisha kata tamaa.

“Jamani tuambiane ukweli, Haji hatopona” alisema kasisi.

“Hata nikifa leo jua sijafa leo mimi nilikufa kitambo sana. Nangoja tu kuzikwa.”

“Una maana gani Haji. Ulikufa kitambo vipi tena?” alimsaili kasisi kwa mshangao.

“Nilikufa zama zile nilipozini kwa mara ya kwanza. Nilikufa zama zile nilipokubali dili ya kumfurahisha mke wa mtu ili awe akinipa pesa. Nilikufa kipindi kile nilipojitosa katika dimbwi la ufuska. Nilikufa kipindi kile nilipozini na mama na mtoto wake. Nilikufa zama zile nilipokuwa siruhusu sketi kupita mbele yangu bila kuitongoza na kutaka kuona kilicho ndani. Nilikufa kipindi kile nilipoacha kuwasikiza wahubiri na kuenda kinyume na kila neno lililoandikwa katika kitabu kitakatifu”

Alianza kufafaruka ghafla tena macho kayakodoa.

“Nilikufa zama zile nilizojiona naumiliki ulimwengu na kila ki….” Mgonjwa wetu hakumalizia kauli yake. Alikata roho.

Alisikika mtu pembeni akisema “Kweli haujakufa leo Haji. Ulikufa kitambo. Leo utazikwa tu”

Misamiati

wakimuasa – kwa kutumaini

Kite – huruma

Ayami – nyingi

Kuwabari – kuwaepuka

Baidi – mbali

Kondeni – shambani

Bwende – kitambaa cha kujifunga kiunoni wakati wa kazi

Vigori – wasichana wanaobaleghe

Kudoya – kupeleleza

Dumaa – asiye Na ufahamu wa Jambo

Taamuli – akili

Ina – uhakika

Akagitagita – akasitasita

Anaganzaganza – anababaika

Koto – Tai

Beuo – dharau