DOKTA KOKU

DOKTA KOKU

Edwin Rutinwa, kijana wa miaka kumi na mitano, aliondoka kwa hatua za polepole kwenye stendi ya mabasi ya Bukoba Mjini muda mfupi tu baada ya kuwasili akitokea Ngara. Kichwani alikuwa na mzigo mzito wa maswali uliomwelemea huku mgandamizo mkubwa wa moyo ukikaribia kukipasua kifua chake. Kwa nini aliambiwa amtafute huyo daktari? Ndio swali lililokuwa na uzito mkubwa. Alitoa kipande cha karatasi mfukoni akakisoma kimoyomoyo, kisha alikirudisha tena mfukoni akaendelea kutembea.

Mwendo wake wa miguu, ulimchukua dakika kumi na tano kutembea umbali wa mita mia saba na hamsini mpaka mbele ya lango la kuingilia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba. Mlinzi mmoja kati ya wawili wa hospitali waliokuwa kwenye kibanda chao, alimuwahi kabla hajalifikia geti dogo la kuingilia ndani.

“Muda wa kuona wagonjwa haujafika,” mlinzi yule alisema huku akimwonesha ishara ya kiganja cha mkono wa kulia aliouinua na kuusukuma mbele kidogo ya kifua chake.

“Shikamo! Nakwenda kwa Dokta Koku,” Edwin alisema huku akisimama.

Sasa mlinzi alitoka kibandani akasogea mpaka getini, akasema huku akimsogelea zaidi, “Marahaba! Una shida gani?”

Edwin alitoa kipande cha karatasi akampa mlinzi lakini hakukipokea. Alikisoma juu kwa juu.

Edwin akamjibu kwa unyenyekevu, “Nimeambiwa nije nikutane naye. Nimetokea Ngara.”

Bila kutia neno jingine, mlinzi alifungua geti dogo akamruhusu aingie. Ewdin alipoingia katika eneo la hospitali akamuuliza mlinzi, “Ofisi yake iko wapi?” Yule mlinzi akamwelekeza.

*** *** ***

Dokta Kokuhumuliza Silvanus Rugarabamu, au Dokta Koku kama alivyoitwa na wengi wakikatisha jina lake, ni Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba. Saa hizo alikuwa hima kutoka ofisini aliposikia mlango wa ofisi yake ukigongwa. Alikwenda kuufungua bila kusema neno akakutana na mvulana amesimama kando ya mlango.

“Karibu,” Dokta Koku alisema akiwa amesimama mlangoni. Mkono wa kushoto alishikilia mlango wakati mkono wa kulia akishikilia mkoba wake mdogo. “Nikusaidie nini?”

“Nina shida ya kuonana na Dokta Koku,” Edwin alisema huku akitoa kipande cha karatasi akamkabidhi.

Dokta Koku alikipokea na kukisoma kwa sauti ya chini, “Dokta Kokuhumuliza Rugarabamu, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba.” Kisha akanyanyua uso kumtazama Ewdin, akasema, “Ni mimi.” Aliufungua zaidi mlango akamkaribisha mgeni wake ofisini. Hapo aliizunguka meza akaketi kwenye kiti chake cha kunesanesa huku akimtaka mgeni wake aketi kwenye kiti kingine kilichowekwa mbele ya meza hiyo. Kabla hajaketi, Edwin alitoa bahasha kwenye kibegi chake akamkabidhi. Dokta Koku aliipokea na kuifungua.

Ndani alitoa karatasi iliyochakaa ikiwa imekunjwa. Ilionesha ilikunjuliwa na kukunjwa mara kwa mara mpaka ikachakaa. Alipoisoma kidogo tu alimtazama mgeni wake kwa mshangao na hapohapo machozi yakamlengalenga machoni mpaka akashindwa kujizuia akalia. Alilia kwa kitambo kifupi halafu alinyamaza akaendelea kusoma. Si kama kilio kilimwishia, la! Alijibembeleza akatulia kwa muda ili aendelee kusoma maana hangaiko la nafsi yake lilidhihiri kadiri alivyosoma karatasi ile.

Kitendo cha Dokta Koku kulia kiliongeza uzito wa maswali kichwani kwa Edwin na ule mgandamizo katika moyo uliongezeka mpaka akaogopa. Sasa maswali mengine makubwa zaidi yaliibuka. Huyu Dokta Koku ni nani? Kwa nini analia baada ya kuisoma barua aliyompa?

Barua ile, Edwin hakuona kama ilitisha au kusikitisha mpaka mtu amwage machozi baada ya kuisoma. Yeye aliisoma mara nyingi sana lakini haikumliza wala kumuogofya. Imekuwaje Dokta Koku analia? Pengine yeye hakuielewa ndio maana haikumliza.

Dokta Koku alikuwa kama yupo kwenye ulimwengu wa pekee. Aliikumbuka sana. Ilikuwa barua aliyoiandika kwa mkono wake kiasi miaka kumi na minne iliyopita. Wakati huo akiwa Ngara akihudumu kama daktari wa magonjwa ya akina mama na watoto katika hospitali ya Murgwanza.

*** *** ***

Miaka kumi na sita iliyopita, Kokuhumuliza Rugarabamu alifika wilayani Ngara katika mkoa wa Kagera akitokea jijini Mwanza. Alifika hapo kufanya kazi ya utabibu katika hospitali ya Murgwanza inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Kagera. Hapo alikuwa akihudumu kama daktari wa magonjwa ya akina mama na watoto.

Siku moja, alipokuwa zamu ya usiku hospitalini hapo alifika mwanamke mjamzito aliyefuatana na mume wake. Baadaye alimfahamu mwanaume kuwa aliitwa Daniel Rutinwa. Mwanamke alifika kwa ajili ya kujifungua. Wawili hao walitokea katika kijiji cha Kanazi. Umbali wa kilomita kumi na moja mpaka hospitalini hapo. Dokta Koku alimpeleka mwanamke kwenye wodi ya wazazi na kumkabidhi kwa wakunga halafu akarudi ofisini kwake.

Muda mfupi tu baada ya kuingia ofisini kwake alipokea taarifa iliyompasua kifua. Mmoja katika wanawake waliojifungua siku hiyo alifikwa na mauti. Taarifa hiyo ilimpasua kifua kwa sababu alimpokea mwanamke huyo kama alivyofanya muda mfupi uliopita.

Ilikuwa saa za jioni katika siku hiyo alipopata habari juu ya mwanamke mjamzito aliyetelekezwa katika mapokezi ya hospitali hiyo. Alipokwenda kumuona alimkuta msichana mdogo aliyemkadiria umri wa miaka kumi na minane. Msichana huyo hakuwa na hali iliyofaa duniani wala ahera. Ujauzito ulimdhoofisha na kumfanya aonekane mgonjwa zaidi. Kwa huruma, dokta Koku alimsaidia kumfikisha kwa wakunga. Baada ya kumfikisha huko aliambiwa hakukuwa na uwezekano wa kujifungua kwa njia ya kawaida kwa kuwa hakuwa na nguvu. Badala yake ilifaa afanyiwe upasuaji ili kunusuru maisha ya mama na mtoto. Taratibu zilipokwisha kukamilika, mwanamke aliingizwa chumba cha upasuaji.

Ripoti ilikuja kwamba msichana alijifungua kwa upasuaji mtoto wa kiume aliyekuwa na afya tele. Lakini tatizo jingine liliripotiwa kwenye dawati la dokta Koku. Upasuaji ulifanikiwa lakini msichana alipoteza damu nyingi, na japo juhudi za kumwongezea damu zilifanywa ilionesha hakuwa na mwendo mrefu katika safari yake ya maisha.

Kwa hivyo, taarifa za kifo cha msichana huyo zilipotua mezani kwake alihuzunika sana. Zaidi alimsikitikia mtoto. Katika siku yake ya kwanza tu duniani alimpoteza mama yake. Jambo baya zaidi msichana yule hakuwa na ndugu aliyejitokeza tangu alipomkuta mapokezi mpaka wakati huo. Wazo moja lilimjia kichwani. Alitoka ofisini mpaka mapokezi.

“Yule msichana uliyeniita nije kumchukua, hakuja na ndugu zake?” Dokta Koku alimuuliza mhudumu wa mapokezi.

“Mimi nilimkuta nilipokuja kuchukua zamu,” mhudumu wa mapokezi alisema akanyamaza. Alipomtazama dokta Koku akaona jinsi alivyofadhaika. Akasema, “Nilimuona amekaa muda mrefu na kulalamika maumivu. Nilipomsemesha hakunijibu ndipo nikakuita wewe. Imekuwaje?”

“Amef… amejifungua kwa upasuaji lakini…” Dokta Koku alipata kigugumizi.

“Amefariki!” Mhudumu wa mapokezi alishtuka.

Dokta Koku alirudi ofisini kwake hali ya kuwa kichwa kikiwaka moto kwa maswali yaliyokosa majibu. Usiku ule ulipita vibaya mno kwake akiwaza jambo la kufanya.

Kulipopambazuka alikwisha kupata wazo la kulitekeleza. Alijithibitishia yeye mwenyewe kwamba, msichana yule hakuwa na ndugu. Na kwa vyovyote atazikwa. Je, mtoto atalelewa na nani au maisha yake yatakuwaje? Hatozikwa pamoja na mama yake angali hai. Kwa hivyo, alitia nia kumchukua akamlee. Alipanga asubuhi hiyo akaufahamishe uongozi wa hospitali juu ya nia yake.

Ilipofika saa mbili asubuhi alijiandaa akatoka ofisini. Mwendo mfupi tu baada ya kutoka ofisini kwake alifuatwa na mmoja wa wauguzi waliokuwa zamu ya usiku katika wodi ya wazazi.

“Dokta, mjamzito uliyemleta usiku amejifungua muda mfupi uliopita lakini mtoto amefariki,” muuguzi alisema. Moyo wa dokta Koku ukatikisika kwa mshtuko. Na mara akajisaili mwenyewe kwamba alikuwa na mkosi gani? Wajawazito wawili aliowapokea usiku uliopita walipata matatizo baada ya kujifungua. Mmoja alifariki baada ya kufanyiwa upasuaji na mwingine alimpoteza mtoto baada ya kujifungua. Alinyamaza kimya kwa muda mrefu akiwaza.

“Alijifungua mtoto gani?” Hatimaye aliuliza.

Muuguzi akamjibu, “Mtoto wa kiume.”

“Mzazi amekwisha kuambiwa?” aliuliza tena.

“Hapana. Amezinduka muda mfupi tu uliopita maana alipoteza fahamu baada ya kujifungua. Hatujamwambia kwa kuhofia kumharibu zaidi. Pia hatujamuona ndugu yake yeyote aliyefika kumjulia hali mpaka sasa,” muuguzi alisema.

Hapo dokta Koku alimsihi muuguzi yule waingie ofisini kwake. Jambo fulani lilimjia kichwani. Walipoingia alimtaka ushauri juu ya nia yake ya kumlea mtoto aliyempoteza mama yake. Juu ya nia hiyo alimweleza namna alivyoona ugumu katika kuutekeleza mpango wake. Mtoto alikuwa mchanga aliyehitaji uangalizi wa karibu na yeye hakuwa na huo muda kutokana na kazi yake. Mbali ya kutakiwa kushika zamu kuwahudumia wagonjwa kulingana na ratiba ya hospitali kulikuwako na miito ya dharura ambayo ingelazimu kumwacha mtoto ili akawajibike. Na dharura hutokea wakati wowote. Itakuwaje iwapo atapata dharura usiku naye aliishi peke yake?

“Unaonaje tukimkabidhi mtoto kwa mama huyu?” muuguzi aliuliza.

“Unadhani itakuwa sahihi?” Dokta Koku aliuliza kwa mashaka.

“Haitakuwa sahihi iwapo atajua analea mtoto asiyekuwa wake. Kama hatojua wala haina shida.”

“Ninalo wazo,” dokta Koku alisema, “Huyu mwanamke alikuja na mume wake. Nadhani hayuko mbali na hapa.”

“Unataka kumwambia juu ya hili?”

“Nimeona nimshirikishe. Hii itaepusha mambo mengi siku za baadaye. Nitamwambia lakini sitamlazimisha. Akikataa nitatafuta njia nyingine ya kumlea mtoto.”

“Katika rai yangu juu ya hili, naona mtu pekee wa kuambiwa ni mwanaume. Tena si kuambiwa kama amri bali kushauriana naye. Sisi wanawake kuna namna tulivyo hasa linapokuja suala la uzazi. Akishajua mwanawe amefariki na amepewa jukumu la kulea mtoto asiyempata kwa uchungu litaibua jambo jingine lisilokuwa la kawaida,” muuguzi alishauri.

“Umesema vizuri sana. Nitamsubiri mume wake nizungumze naye,” dokta Koku alisema na kunyamaza. Baada ya kimya kifupi alimuomba muuguzi arudi wodini na kumwambia, “Kama atafika mtu na kujitambulisha kwa jina la Daniel Rutinwa mwelekeze ofisini kwangu.”

Baada ya kupita dakika kumi na tano tangu muuguzi kutoka ofisini kwa dokta Koku, mtu mmoja mwanaume aliingia.

“Habari yako, dokta?” Daniel Rutinwa alimsalimia dokta Koku baada ya kumkaribisha kwenye kiti.

“Nzuri sana bwana Rutinwa. Habari ya tangu jana?”

“Salama, dokta. Nilifika kwenye wodi ya wazazi lakini nimeambiwa nije huku kwanza,” Daniel Rutinwa alisema. Dokta Koku akahisi baridi kali iliyomwingia mpaka tumboni. Ni yeye aliyeomba kukutana naye lakini mpaka wakati huo hakupata maneno aliyodhani yangeanzisha mazungumzo baada ya ile salamu.

“Ndio…” dokta Koku alianza kusema na kabla hajaendelea alinyamaza akatazama kando kutafuta ujasiri. Alivuta pumzi kwa nguvu kisha akamtazama mgeni wake. Akasema, “Mke wako amejifungua alfajiri ya leo lakini mtoto hakuishi.”

Mwili wa Daniel Rutinwa ukaishiwa nguvu baada ya kuambiwa hivyo. Furaha aliyoamka nayo akiamini alikuwa baba ilipotea ghafla. Fikra kwamba amekosa mrithi wa jina la ukoo wake zilimfanya amwage machozi na kuiwazia idhilali atakayopambana nayo mke wake kutoka kwa wifi zake. Katika miaka mitano ya ndoa yao, maneno na kejeli za dada zake zilikoma miezi tisa iliyopita baada ya kubaini mke wake alishika ujauzito. Kabla ya hapo, dada zake walimsakama mno kwa maneno ya kukera na kebehi wakimwambia alikuwa anakula chakula cha bure kujaza choo kwa sababu hakushika ujauzito. Sasa mtoto amefariki hata kabla hajamshika mikononi. Itakuwaje?

“Mke wangu anaendeleaje?” Daniel Rutinwa aliuliza baada ya kupoza moyo. Dokta Koku ambaye alikuwa kimya muda wote akimsikitikia, alinyanyua uso akamtazama moja kwa moja kwenye macho.

Akamwambia, “Yuko salama. Japo alipoteza fahamu baada ya kujifungua. Nimehakikishiwa yupo vizuri kabisa.”

“Anajua kama hajapata nafasi ya kumlea mwanawe?”

“Hajaambiwa na ndio maana niliomba kukutana na wewe kabla hujakwenda kumuona.”

“Ni haki yake kujua. Mimi sitaweza kumwambia maana ataumia zaidi. Unajua…” Daniel Rutinwa alisema, “Kupata au kutopata mtoto ni mamlaka ya Mwenyezi Mungu, lakini ndugu zangu hawalitambui hilo. Kila mara wamekuwa wakimsema mke wangu kwa maneno ya ovyo na kejeli. Aliposhika ujauzito alifurahi sana akiamini ataishi kwa amani baada ya hapo. Tukio hili litamvunja moyo kabisa.”

Simulizi fupi ya Daniel Rutinwa ilimhuzunisha sana dokta Koku. Alimtazama kwa macho yaliyojaa huruma. Hata hivyo, alimsihi atulie na awe tayari kumsikiliza. Daniel Rutinwa alipotulia, dokta Koku akamsimulia kisa cha msichana mjamzito aliyetelekezwa mapokezi na jinsi alivyopoteza maisha baada ya upasuaji ulionusuru uhai wa mtoto.

“Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekuja kuulizia juu ya msichana yule. Hatma ya mama imekwisha kujulikana. Amefariki na atazikwa. Vipi kuhusu mtoto? Azikwe angali hai au zitumike mbinu zisizofaa kukatisha uhai wake kwa kuwa hakuna atakayemlea?” alihoji.

Daniel Rutinwa alinyamaza kimya. Dokta Koku akaendelea, “Nimetia nia ya kumchukua nikamlee. Lakini, kuna ugumu katika kulitekeleza hilo kulingana na kazi yangu. Tukio hili limetokea ghalfa na mimi ninaishi peke yangu. Na, kama ujuavyo, mtoto mdogo anahitaji uangalizi wa karibu sana. Kwa hivyo, nimeona tushirikiane kwa pamoja kumlea huyu mtoto.”

Daniel Rutinwa alipumua kwa nguvu huku akinyanyua uso wake kutazama kwenye dari. Mtihani mkubwa ulikuwa mbele yake. Alikwenda hospitalini pale akijua atarudi na mtoto aliyetoka kwenye mgongo wake. Hata hivyo, jitihada hazishindi kudura. Mche wa mbegu aliyoipanda na kuimwagilia maji kwa muda mrefu ulikufa muda mfupi tu baada ya kuchomoza ardhini. Na sasa alitiwa kwenye mtihani wa kuutunza mche uliochomoza ardhini lakini hakushiriki kuipanda wala kuimwagilia maji mbegu yake.

Mbali na hayo, alimpenda sana mke wake na aliumizwa na visa vya dada zake. Kufa kwa mche wake ilimaanisha visa vitaibuka upya na haikosi watasema hakuwa na ujauzito bali alisingizia tu kupoza hasira zao. Alikata shauri kukubali rai ya dokta Koku ili kumnusuru mke wake japokuwa alitakiwa kuamua kwa busara.

“Naamini hii hatokuwa faraja kama uliyoitarajia. Lakini, tazamia jaza yako kutoka kwa Mwenyezi Mungu ukiyafanya malezi ya mtoto kuwa sadaka.” Daniel Rutinwa aliibuliwa na dokta Koku kutoka kwenye kina kirefu cha bahari ya mawazo.

“Nimekuelewa, dokta,” Daniel Rutinwa alisema, “Nitamchukua lakini kwa sharti moja. Mke wangu asijue kama mwana si wake ili amlee vizuri.”

Maneno hayo yalimpa faraja dokta Koku. Makubaliano yalifanywa baina yao kwamba Daniel Rutinwa atakuwa na haki zote kwa mtoto kama baba mzazi lakini akishrikiana kwa siri na dokta Koku katika kumlea. Dokta Koku aliahidi kushughulikia mambo yote yaliyohusu matibabu na alimuomba Rutinwa kufika hospitalini hapo mara kwa mara kuona maendeleo ya mtoto. Kiapo kuificha siri hiyo kwa mke wa Rutinwa kilifanywa kwa siri pia.

Daniel Rutinwa na mke wake waliruhusiwa kuduri nyumbani baada ya kukabidhiwa mtoto wao waliyemwita Edwin Rutinwa.

Utekelezaji wa ahadi haukuwa kitu kwa Daniel Rutinwa. Mara kwa mara alifika hospitali akiwa na mke kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya mtoto wao. Na baadaye alikutana na dokta Koku wakapanga zaidi juu ya malezi ya mtoto.

Miezi mitatu kabla mtoto Edwin Rutinwa hajatimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa, dokta Koku alipata wito wa dharura akaenda Kigoma kujumuika na madaktari wa shirika la kimataifa kutoa huduma za kitabibu kwa wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu.

Miezi minne baadaye alirudi Ngara kufuata vifaa vilivyotumwa na alitakiwa kuwa huko kwa wiki moja tu kisha arudi Kigoma kuendelea kazi ya utabibu. Alipofika hospitali aliambiwa mtu aliyeitwa Daniel Rutinwa alifika pale mara kwa mara. Pamoja na mambo mengine yaliyomfikisha aliambiwa kuwa alimuulizia sana. Alifurahi sana kusikia hivyo, na japo alitamani kukutana naye lakini hakuwa na muda mrefu wa kukaa Ngara. Alitakiwa afanye alichokiendea kisha arudi Kigoma. Kitu alichofikiria kukifanya kwa wakati huo ni kumwachia Daniel Rutinwa ujumbe. Alichukua kalamu na karatasi akaandika barua.

Kwa

Ndugu Daniel Rutinwa wa Kijiji cha Kanazi, Ngara.

Natumaini mnaendelea vizuri wewe na familia yako.

Nimefurahi sana kusikia ulikuja hospitali kufuatilia maendeleo ya afya ya mtoto. Mimi nilipata safari ya dharura kwenda kuwashughulikia wagonjwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma. Na hata hapa nikuandikiapo barua hii nimekuja Ngara mara moja tu kufuata baadhi ya vifaa halafu nitarejea tena Kigoma. Kwa hivyo, nimeona nikuandikie kukujulisha maana sitapata wakati wa kukutembelea kijijini kwako japo nilipenda iwe hivyo.

Nimefarijika sana kuona mtoto ametimiza umri wa mwaka mmoja na anaendelea vyema kiafya. Hii inanipa imani na matumaini makubwa kwamba unatunza ahadi yako.

Nitakuandikia tena nitakaporudi Ngara ili ufike ofisini tujadili namna gani tunaweza kushirikiana zaidi katika kumtunza mtoto.

Wasalaam,

Dkt. Kokuhumuliza Rugarabamu,

Ngara.

Alipokwisha kuiandika aliicha kwa daktari aliyekaimu nafasi yake akimtaka aikabidhi kwa Daniel Rutinwa siku atakayofika kufuatilia maendeleo ya mtoto kisha yeye alirudi Kigoma alikoishi kwa miaka mitatu. Baadaye alirudi Ngara kukabidhi ofisi maana alipata uhamisho kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba alikohudumu kwa miaka saba kabla ya kuteuliwa kuwa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo.

*** *** ***

“Mbona umekuja peke yako? Baba yako yuko wapi?” hatimaye dokta Koku alimuuliza Edwin baada ya kumaliza kusoma barua.

“Baba amefariki,” Edwin alijibu huku akigeuza shingo kutazama pembeni. Mshindo mwingine usiokuwa wa kawaida ulikita katika moyo wa dokta Koku na yowe kubwa la kilio cha uchungu likamtoka. Mtu aliyepanga naye mipango na kuwekeana ahadi ya malezi ya mtoto alimaliza mwendo katika safari yake ya maisha. Pengine hilo halikumuumiza sana maana kifo ni desturi katika mapito ya binadamu. Kilichomuumiza ni kutokuwa na mawasiliano naye tangu alipomwandikia barua ambayo sasa ilirudi tena mikononi mwake. Hakujua mtoto Edwin aliendeleaje katika makuzi yake na alipitia changamoto zipi. Hata hivyo, alimshukuru Mungu mtoto aliyemkabidhi akiwa kichanga alikuwa mbele yake akiwa mkubwa.

Aliponyamaza kulia na kufuta machozi akamuuliza tena kwa sauti ya upole, “Na mama anaendeleaje?” Jibu alilopewa lilimnyanyua kwenye kiti akaenda kumkumbatia Edwin kwa upendo na huruma. Alipomuachia na kurudi kwenye kiti chake alimuomba amsimulie japo kidogo kuhusu maisha yake.

Edwin akasimulia kwamba, siku moja alipokuwa darasa la sita baba yake alirudi nyumbani akiwa amechoka sana na mwenye mawazo. Hiyo ilikuwa baada ya kutoweka nyumbani kwa wiki nzima. Baada ya kusalimiana naye alimuomba kalamu na karatasi. Alipompa aliingia chumbani kwake na baadaye alitoka akiwa na karatasi mbili; moja aliikunja akamshikisha mkono wa kushoto. Karatasi nyingine alimshikisha mkono wa kulia akamwambia aisome palepale.

Nenda Hospitali ya Murgwanza ukamuulizie dokta Kokuhumuliza Rugarabamu. Hakikisha unampata na umpatie hiyo barua.

“Alichukua begi akaingia chumbani kwangu akatia nguo na kunipa. Alinipa kiasi cha fedha akaniambia niondoke na nisirudi mpaka nitakapompata dokta Koku. Nilipotoka tu nyumba yetu iliwaka moto. Baba na mama hawakutoka. Nilipofika Murgwanza niliambiwa dokta Koku amehama. Nikapewa hicho kikaratasi kilichonifikisha hapa.” Edwin alimaliza kusimulia.

Simulizi ilikuwa fupi lakini ilitosha kuuchana moyo wa dokta Koku. Alimfikiria Daniel Rutinwa akaona vita kubwa aliyoipigana mpaka kufikia hatua ya kuchoma moto nyumba yake. Hakuwa na shaka kwamba siri waliyoapa kuificha ilifichuka. Alipomtazama Edwin hakuona kama alifanana na mtu yeyote katika watu aliopata kuwaona. Alisimama na kumuashiria Edwin naye asimame. Akamwambia, “Mimi ni shangazi yako. Na kuanzia sasa utaishi na mimi katika hali zote.” Alimshika mkono akamuongoza kutoka ofisini.