Kaa la moto

Kaa la moto

Upande wa kushoto alisimama mwanamke mmoja mwenye kimo kirefu na rangi ya ngozi yake ni nyeusi tii! Mbele yake alisimama mwanaume naye akiwa na kimo kirefu na hata rangi ya ngozi yake ni nyeusi. Umri wao haujapishana sana. Ni kati ya miaka thalathini na thalathini na mitano lakini mwanaume akionekana kumzidi mwanamke.

Katikati yao palikuwa na wanawake wawili: mama mtu-mzima ambaye umri wake ulifikia miaka sitini au sitini na tano. Naye, japo alikuwa amekaa kwenye mkeka, kimo chake kilionekana kuwa kirefu na ngozi yake ni nyeusi kama wale waliosimama. Pamoja naye pale mkekani alikuwako mwanamke mwingine aliyeonekana kuwa na umri wa chini ya miaka thelathini. Mwanamke huyo aliyekuwa na sura ya upole, alizungukwa na watoto watatu—mmoja wa kiume na wawili wa kike. Wakati watoto wa kike wakimkumbatia mama yao, yule wa kiume alikuwa amemuegamia begani.

Nilipofika karibu yao, nikawasalimu, “Habari zenu!” ndio desturi za kiungwana zilivyo. Ukikuta mtu au watu, basi wajulie hali halafu uendelee na mambo mengine.

Lakini, licha ya kuwaonesha uungwana wangu, ni mmoja tu kati yao aliitikia salamu yangu. Naye ni yule mwanamke mtu-mzima, ambaye hata hivyo, aliitikia bila kurudisha salamu na tena akionekana kutopenda kitendo changu kile. Aliitikia tu “Nzuri,” huku akinitazama kwa jisho la pembeni.

Kitendo cha kunitazama kwa jicho la pembeni ndicho hasa kilinifanya nisimame, maana kiliniudhi sana. Niliona kuwa amenidharau, na afadhali na yeye angeinyamazia tu salamu yangu kuliko kuijibu na kunitazama namna ile kama nilikuwa kitu kisichostahili tazamo lake.

Basi, kabla sijamrushia maneno ya kuudhi yule mama mtu-mzima, macho yangu yalitua kwa mwanamke aliyekaa pembeni yake akiwa na watoto nikaona akilia kwa kwikwi na machozi yakimwagika kama bomba la maji lililopasuka. Watoto nao, hasa wa kike walilia pamoja naye. Nadhani walilia tu kwa umuona mama yao akilia bila kujua kilichokuwa kikimliza.

“Vipi jamani, kuna msiba?” nilijikuta nikuliza macho yangu yangali bado kwa mwanamke yule.

“Hayakuhusu,” alidakia yule mwanamke mrefu aliyekuwa amesimama tena kwa hasira na akinitupia jicho la kunionya. Bila kujua, jibu lile lilinipa nguvu ya kutaka kujua kilichoendelea pale. Niliona hapakuwa na jambo la kawaida na tena nikajiuliza iweje anayelia ni mmoja tu na wale wengine, japo hawakuwa na huzuni lakini sura zao zilionesha chuki. Kuna nini? Nilijipiga swali.

Nilisogea karibu zaidi nipate kumuona vyema yule mwanamke mwenye watoto na mara kumbukumbu ilinijia. Nilimuona makaburini akiwa na watoto wake vilevile. Ilikuwa siku tuliyokwenda kumzika mwanaume mmoja aliyeanguka na gari akafa papo hapo. Ilinijia tu akilini siku hiyo, baada ya kumuona akiomboleza kwa uchungu na huku amewakumbatia wanae, ya kuwa, tuliyekuwa tukimzika alikuwa mume wake. Na hata watu wale wengine, hasa mama mtu-mzima na mwanamke aliyesimama, niliwaona wakibembelezana japo sikuwazingatia wakati ule. Miezi mitatu ilikuwa imepita tangu tukio hilo.

“Habari yako dada?” nilimwinamia nikamshika kidevu na kuinua kichwa chake tupate kutazamana.

“Nzuri kaka yangu,” mwanamke alijibu huku akijitahidi kufuta macho za mkono wa fulana yake ya mikono mirefu.

“Kulikoni? Mbona unalia peke yako?” nilimtupia maswali mfululizo bila kujali wale wengine watanionaje.

Maswali yangu hayo yalimwinamisha yule mwanamke aliyekuwa amesimama akanishika ukosi wa shati langu na kuniinua kwa ghadhabu huku akinitupia maneno makali, “Nimekwambia hayakuhusu. We’ vipi? Nenda na safari yako.” Kwa sababu ya kuwa mwili wangu mdogo na japo nilikuwa nimemzidi umri, alinikusanya kama kiroba cha takataka akanitupia huko.

Niliinuka nikarudi mahali pale nami nikiwa nimeghadhibika sana. Kulikuwa na nini mpaka anifanyie vile? Nilipowafikia kwa mara nyingine, nilimtazama usoni yule mwanamke ambaye sasa aliikusanya kanga yake akajifunga kiuoni. Wakati huo, Yule mwanaume alisogea mbele akanizuia nisimfikie yule mwanamke mwenye watoto.

“Bwana, umeshapewa onyo. Hapa hapakufai,” aliniambia huku akitaka kunishika mabega lakini niliipangusa mikono yake kwa nguvu mpaka akashtuka. Na yule mwanamke aliyekuwa tayari kunishughulikia, alitulia na huku akipumua kwa hasira.

“Eti dada yangu…” nilimgeukia yule mwanamke mwenye watoto. Naye ananiangalia usoni kwa macho yaliyojaa machozi. Macho yenye kusema jambo fulani na yanayobembeleza na kuomba msaada. “…kuna nini?” nilimuuliza.

“Huyu…” alisema huku akimnyooshea kidole mwanamke aliyekuwa amesimama na ambaye wakati huo aligeuka ghafla kumtazama yule mwanamke mwenye watoto kwa macho makali akamtaka anyamaze kwa kumfanyia ishara ya kidole cha shahada alichokiweka mdomoni, “..ni wifi yangu. Na huyu…” mwanamke mwenye watoto aliendelea bila kujali karipio la kumtaka akae kimya. Sasa alimnyooshea kidole mwanaume aliyesimama mbele yangu, “…ni shemeji yangu.” Alinyamaza akanitazama usoni nami nikatikisa kichwa kumtaka aendelee.

“Na huyu,” aliendelea kusema huku akimshika bega mama mtu-mzima ambaye aliupangusa mkono huo kama ambaye alimpangusa mdudu mwenye sumu kali, “…ni mama mkwe wangu.”

“Ndio! Tatizo liko wapi?” niliitikia kumkubalia utambulisho wake na kumuuliza kwa wakati mmoja.

“Wanataka niwape funguo za nyumba; kadi ya benki na hati ya shamba alivyoviwacha marehemu mume wangu—baba wa hawa watoto,” alisema na kuanza kulia tena, “Mi’ n’taishi vipi na hawa watoto?”

“Ndioo!” mwanamke mrefu anadakia kwa sauti ya juu, “Tena unatuchelewesha tu hapa. Hizo mali hazikuhu ni zetu. Mali ya kaka yetu. We’ hukuja na kitu hapa unaving’ang’ania tu.” Mapovu yanamtoka kwenye pembe za mdomo wake.

Sijawahi kuona mwanamke alokosa haya katika maisha yangu kama huyu. Najisemea huku nikimtazama kwa hasira. ningekuwa na uwezo ningemkatakata vipande nikawatupia mbwa wamle.

“Shem,” mwanaume anaunganisha maneno ya dada yake, “Unatuchelewesha ujue. Tuna mambo mengi ya kufanya sio tunatazamana tu hapa.”

Maneno yake yananifanya niangue kicheko. Japokuwa nilishindwa kukizuia kicheko changu, jambo lile halikuwa la kuchekesha. Lilikuwa mojawapo ya mambo ya kuchukiza sana na kutia hasia na niliona linayazidi mambo yote ya kuchukiza duniani. Ndio maana niliambiwa hayanihusu. Nilijiambia mawazoni. Hata hivyo, hayakunihusu kweli. Nilijitia vishindo tu kama mpangaji kutunishiana misuli na mwenye nyumba lakini mwisho wa siku alihama akamuacha mwenye nyumba.

Ndio yaliyonikuta mimi. Hata hivyo, sikukubali mambo yale yasinihusu moja kwa moja. Nilijikohoza kimamlaka nikasema kwa kujiamini, “Sikiliza dada yangu…” yule mwanamke aliinua uso akanitazama kwa kunisihi nisimuache peke yake wasije kumla nyama na watu wale waliokuwa na roho mbaya.

“…haya mambo hayanihusu, lakini…” nilisema na kabla sijaendelea yule alinikata kauli, “Nenda bwana. Nani amekuita hapa?” Alinijia kwa kasi alipoona simjali lakini alisimama ghafla aliposikia nikisema, “Kachukue hizo funguo za nyumba, na hiyo hati ya shamba na kadi ya benki na vyeti vya kuzaliwa vya watoto.” Nilinyamaza nikawa nawatazama kwa zamu. Wote waliokuwako pale walinitazama usoni wakiwa wameshangaa.

“Katika maelezo yako sijasikia kama wanawataka na watoto waondoke nao,” niliendelea kusema huku nikimtazama zaidi mwanamke mwenye watoto, “Lakini kwa sababu wanataka vitu vya kaka yao, basi hata hawa watoto ni mali yao. Maana we’ hukuja na kitu kama alivyosema wifi yako.” Niliposema hivyo nikawaona watu wale wakiishiwa nguvu.

“Wewe wala usiwe na wasiwasi,” nilimfuata mwanamke mwenye watoto nikamshika mabega, “Vitu vyote vya ndugu yao waachie, labda uondoke na begi lako la nguo tu kama siku uliyokuja. Mtoto mmoja atakwenda kwa shangazi lake; mwingine ataishi na baba yake mdogo na atayebaki ataishi na bibi yake…” kabla sijamaliza, nikamuona mwanamke mrefu akifungua kanga aliyokuwa amejifunga kiunoni alipotaka kupambana na mimi akajitanda kichwani na huku akitoa simu kwenye mfuko wa dera na kuiweka sikioni.

“Hallo!” alisema, lakini nikaanza kucheka baada ya simu ile kuanza kuitia mara tu alipoibandika sikioni. “Hapa network ni shida sana,” alijisema kwa sauti ya chini na huku akisogea mbali na eneo lile.

Wakati mwanamke akiondoka, nilisikia sauti ya mwanaume akijihoza na kutema mate na kufukia huku akipiga hatua kwenda mbele polepoleu. Ikawa anajikohoza na kutema tema tu mate na huku anasonga mbele bila kugeuka. Niliendelea kumtazama akienda zake, na nilipogeuka, nikamuona mama mtu-mzima, akiwa amesimama wima na simu ameibandika sikioni, “Vikoba vimeanza? Haya nakuja,” alisema huku akiiruhusu miguu yake itengeneze hatua akaenda zake.

Pale nilibakia mimi na mwanamke mwenye watoto na watoto wake. Wengine walitawanyika kila mmoja uelekeo wake. Mmoja alikwenda kutafuta network, mwingine anachimba na kufukia mchanga kwa miguu yake na kutema mate. Na mwingine anawahi kwenye vikoba.