Neno La Mwisho

Ramadhan Makoleko

Kwako mwanangu mpenzi;

Natumaini uko salama!

Mwanangu, nilitamani siku moja nikuone ili angalau nikusimulie kuhusu mambo ya ulimwengu ambayo mimi nilipata kuyaona. Nikusimulie kuhusu vita vilivyowahi kupiganwa na mashujaa; nikusimulie juu ya shida za ulimwengu, nikuhadithie kuhusu dhiki zilizowahi kuwapata walimwengu, nikuambie kuhusu taabu za mababu, nikudokeze matatizo na faraja zilizowahi kutawala ulimwenguni. Nikusimulie kuhusu tawala na watawala wake. Nikuhabarishe juu ya Wafalme na Malkia na wanamfalme na majemedari na wababe waliowahi kukanyaga na kuacha alama kwenye mgongo wa ardhi hii.

Mwanangu;

Nilipokuwa nikiandika neno hili, nilimuusia mama yako, wakati huo akiwa na mimba iliyokubeba wewe, ya kuwa, atakapojifungua, akuite jina zuri ambalo ama halikuwahi kuitwa kokote duniani au asikuite jina kabisa. Kwa sababu, nilitumaini jina ningekuita mimi mwenyewe. Nilitaka nikutafutie jina litakaloendana nawe na liwe mfano kwa watu wengine. Yapo majina mengi sana ya watawala wa kale na majemedari wa vita na watu wengine mashuhuri waliowahi kuishi na kutenda mambo makubwa ambayo yamekuwa yakipigiwa mfano mpaka sasa. Nilitaka jina lako liwe kama watu hao.

Kuna majina ya wanyama wazuri wenye sifa anuai; wenye nguvu na werevu ambao wazazi wamekuwa wakiwaita watoto wao. Na wapo ndege wazuri wenye rangi zinazovutia tazamo la kila mtu na wenye maumbo mazuri na majina yatiayo ladha ulimini mwa mtamkaji.

Lakini, juu ya hayo, sikuona ambalo lingechukuana moja kwa moja na wewe. Iwe ama kutoka kwa wanyama; au ndege, au miti au watawala na majemedari wao. Japokuwa sijaiona sura yako, ni hakika ya moyo wangu kwamba umekuwa na sura ileile kama niliyooneshwa kwenye ndoto niliyowahi kuota kabla mimba yako kutunga. Kwa hivyo, nilitaka pia jina lako liendane na wajihi na siha yako ili kila akutafutaye ama mchana au usiku akuone kwa wepesi.

Mwanangu;

Nasikitika sikupata nafasi ya kuiona sura yako kwa sababu ya safari iliyonipata ghafla mwezi mmoja kuelekea uzazi wako. Safari yangu ni ndefu ambayo sitarajii kurudi kesho wala keshokutwa. Maana mpaka sasa sijafika niendako wala sina hakika kama nimefika hata nusu yake. Fanya hesabu, tangu mwezi mmoja kabla hujazaliwa mpaka sasa na umri wako huo, ni miaka mingapi imepita? Sasa, katika miaka yote hiyo iwe sijafika hata nusu usifikiri itakuwa safari fupi itakayonirudisha nyumbani miaka ya karibuni.

Hata hivyo, safari yangu japo ilikuwa ya ghafla nilijiapiza kwamba nisingesafiri hata mwendo wa hatua tano bila kukuachia neno ili likufae katika maisha yako wewe pamoja na aali zako. Natazamia neno langu litakuwa ishara ya matumaini na ukunjufu. Kwa hivyo, sidhani kama utalitupa likaenda bure kama taka zichukuliwavyo na mkondo wa maji ya mto. Chonde usiogope wala kushtuka maana hivi ni namna mzazi yeyote hufanya kwa mwanawe. Nataka ujifunze kila mara usomapo neno hili maana mja hajui yote. Yaliyopo utayaishi na yaliyopita utajifunza kwa walioyaishi.

Mwanangu;

Kama ilivyo miguu miwili, au macho mawili, au mikono miwili na, au masikio mawili kwa binadamu, vilevile johari za mja ni mbili tu; akili na soni. Vitu hivi havijawahi kuachana na havitaachana. Mfano wake ni kama pande mbili za sarafu moja—upande mmoja hukosa thamani ukikosekana upande mwingine. Kwa hivyo, mtu akiwa na akili hakosi soni na kinyume chake: mtu mwenye soni ni muhali kukosa akili. Nimetaka neno hili likufike kwanza kabla ya neno jengine linalofuatia ili iwe rahisi kwako kuzingatia. Japokuwa sijakutia machoni mwangu, ninayo hakika johari hizi unazo.

Akili itakusaidia kupambanua mambo na kuyatengea muda wa kuyaendea. Akili itakujuza watu na mienendo yao na itakupa mwangaza na utambuzi wa kila jambo isipokuwa lile lililofichwa nje ya uwezo wako. Akili ndio itakuwezesha kuchora mstari kutenganisha baina ya ukweli na uongo; haki na batili, halali na haramu, unyenyekevu na woga, na uungwana na utwana.

Lakini soni itakukataza kufanya kila jambo na itakuzuia kuona kila kitu kuwa ni sawa au sahihi. Soni itakubainishia adabu katika uso wa mtu na itakuonesha utu ndani ya nafsi ya mtu na itakusogezea heshima na kukupeleka kwenye uadilifu.

Mwanangu;

Ulimwengu umebadilika na umekuwa kama nungunungu. Chondechonde uuendee kwa tahadhari usiupige pambaja. Pamoja na hayo, mabadiliko hayo yasikuchote kifikra yakakutoa akili ukabaki na kichwa kitupu kama nyumba iliyoezuliwa paa. Umejaaliwa maisha na usiache kuishi kulingana na wakati wako. Maisha ni hidaya, maisha ni tajamala. Sisi—mimi na mama yako, tumekutengenezea maisha na kwa hivyo, wajibu wetu kwako umetimizwa japokuwa hatuwezi kubadili majaaliwa. Jukumu lako sasa ni kuishi maisha yako.

Katika kuishi kwako, yapo mengi utakabiliana nayo; utaumia, utahuzunika na utahangaika na wakati mwingine kuhangaishwa. Usikate tamaa. Mtu anayekata tamaa huzuia hatima yake yeye mwenyewe. Maisha kwa binadamu hayajafanywa kuwa rahisi wala magumu. Ni mtu yeye mwenyewe huamua jinsi ya kuishi—ama ayafanye maisha yake kuwa rahisi au ajichagulie maisha magumu. Wewe usiyafanye maisha yako kuwa magumu wala usiyarahisishe. lifuate kila jambo kwa wakati wake. Hakuna njia fupi katika kuishi, na ipo kanuni kwamba jambo moja hufanywa baada ya jingine. Ni kusema kwamba, baada ya kitako ni dede na baadaye tete, si kukimbia.

Vaa jaramandia la silaha upigane sawasawa vita vya ukata na ujinga na upambane kufa na kupona ili uendelee kuishi mpaka pale itakapokufikia hatima yako. Hapo hautakuwa na chaguo. Jambo la muhimu ni kutafuta suluhu kila unapokwama. Ukikwama jikwamue na ukikwamishwa pia jikwamue kwa juhudi zako. Watu wanaweza kukukwamishwa na usipojikwamua hakuna atakayekukwamua. Tamthili ya jambo hili ni kama jeraha. Unaweza kujeruhiwa na mtu pengine kwa makusudi lakini kuliponya jeraha hilo ni jukumu lako.

Mwanangu;

Mabadiliko ya nyakati katika ulimwengu, yamefanya mambo yasiyofaa kuonekana kuwa yanafaa. Haramu imehalalishwa kuwa halali mpaka kamari imebadilishwa jina na ndio hiyo unayosikia ikiitwa bahati nasibu na majina mengine mazuri ili kuipendezesha iwavutie watu. Inalipiwa kodi na kupewa kibali kuihalalisha. Lakini nikwambie, japokuwa inapambwa sana, hiyo ni dhulma na wizi uliokuwa mkubwa. Mfano wake ni kama punda na pundamilia. Ukimpaka rangi punda ili aonekane kama pundamilia haitamaanisha kuwa amekuwa pundamilia. Rangi haitafaa kuwalinganisha hata wakiwekwa pamoja maana tabia zao ni tofauti. Ndio halali na haramu zilivyo.

Mtu muungwana husifika kwa chumo lake la halali na haki. Mtu bora ni anayemwagika jasho kwa ajili ya kuishi kwake kuliko mtu anayeishi kwa jasho la mwingine. Usije ukasema hata kamari hiyo au niseme bahati nasibu umecheza kwa jasho lako na kwamba huoni vibaya ukiishi kwa jambo hilo. Ngoja nikuambie jambo jingine, mtu huvuna alipopanda au hulipwa kulingana na kazi aliyoifanya. Ukiona unavuna zaidi ya ulichopanda au kulipwa zaidi ya kazi uliyofanya, jitazame sana. Haikosi utakuwa unakula chumo la mtu mwingine. Na je, huoni kama utakuwa umedhulumu?

Anayelima huvuna na afanyaye kazi huona ijara ya kazi. Huko kwingine ni mtu mmoja au watu wawili au watu watatu, au watu wanne ndio hubahatika katika kundi la watu mia elfu waliobahatisha japokuwa wote walitaka kubahatika. Hapo utagundua waliokosa ndio wamekuchangia ukapata milioni kwa elfu moja yako. Ulipata kuona wapi mtu akatoa elfu moja akapata milioni moja kwa kusema tu fulani atapigwa? Au timu fulani itafungwa? Je, huoni kama umedhulumu? Katika kukuongezea maarifa nitakuambia jambo jingine, dhuluma haiendi moja kwa moja kama maji kwenye mkondo wa mto au bahari. Dhuluma ikienda inarudi. Mfano wake ni kama ubaya: ukitenda ubaya hautalipwa wema ndivyo dhuluma ilivyo. Ukidhulumu nawe utadhulumiwa.

Mwanangu;

Njia unayosikia sasa ikiitwa mapenzi, miaka ya zamani ilikuwa inaitwa zinaa. Hilo ndio jina halisi. Ni moja katika njia mbaya mno ambayo haimfikishi anayepita isipokuwa kwenye maangamizo na majuto. Imebadilishwa na kuitwa jina hilo ili kuwavutia watu waiendee. Chonde, chombo utakachokichagua kusafiria katika safari ya maisha yako, hakikisha hakipiti kwenye njia hiyo. Kuna watu katika maisha watakuambia unakosa raha za ulimwengu kwa kuwa hupiti kwenye njia hiyo. Hakuna raha inayoishia kwenye majuto au maangamizo. Raha huanza kwa raha na huisha kwa raha. Raha isiyoanza wala kuisha kwa raha si raha ni karaha.

Njia hiyo, imewapoteza watu wengi sana. Kuna watu wameyadharau mpaka maisha yao wenyewe kwa kupoteza furaha na kuacha kutenda wajibu wao na mengine mengi waliyopaswa kuyatenda.

Mwanangu;

Zamani, ilifahamika mwenzawazimu ndio mtu pekee awezaye kwenda uchi barabarani. Na japo iliaminika hivyo, ilikuwa aghalabu kukutana na mwendawazimu akiwa katika hali hiyo. Kila alipoonekana alivishwa nguo maana ilitia kiwi cha macho kuona utupu wa mtu mwingine. Lakini siku hizi imekuwa tofauti sana. Kwenda uchi barabarani imekuwa fasheni na watu wamekuwa wakijifaharisha kwa kuonesha maungo yao hadharani. Anayekaa na kutembea uchi mbele ya watu hutajwa kuwa mrimbwende na hodari katika fasheni na mitindo na hutuzwa kwa mataji na pesa.

Mwanangu, wewe ni heshima na kielelezo cha ukoo wetu wote. Wewe ni hadhi katika utajo wetu wote—kuanzia kwa mababu mpaka sasa. Wewe ni fahari ya mila, tamaduni na desturi yetu itakayodumu katika vizazi vingi. Usitembee bila kusitiri mwili wako.

Wakati ule naandika neno hii, nilimwambia mama yako, na nilikuwa nikiweka msisitizo kila mara kwamba, akuelekeze nguo za kuvaa na namna ya kuvaa lakini nilimkataza asikuchagulie mavazi. Na sasa nakariri kauli yangu kwenye neno hili, asikuchagulie nguo. Narudia tena, asikuchagulie nguo. Moja ya majukumu yangu mimi baba yako kama ningekuwa karibu nawe, ningehakikisha nayajua mavazi yako. Kwa hivyo, ni wajibu wa mama yako sasa kuhakikisha anajua umevaa nini sio kukuchagulia utakachovaa.

Mwanangu;

Ulimwenguni, usihangaike kutaka kuwajua watu kwanza ili uwapende au wakupende. Utakuwa umetenda dhambi kubwa sana. Ulimwengu ni tajiri-mchoyo. Hudhihirisha machache tu na kuficha mengi. Ulimwengu unaweza kukupa watu ukakuficha tabia na mienendo yao.

Kutaka kumjua mtu unahitaji miaka mingi ya kuishi kuliko idadi ya nywele kichwani mwako. Kamwe, usijaribu kutenga muda kutafuta vitabu, makala, majarida, filamu, wala nyimbo na hotuba za watu wanaofundisha mandhari za watu ili upendane nao. Binadamu ni kama ganda la kitabu. Picha ya nje inatafsiriwa na maelezo mengi ya ndani lakini picha utakayoipata kwa maelezo hayo husaidifiana mara chache na ganda la kitabu. Sasa utasoma vitabu vingapi ili umjue mtu na upendane naye?

Kuna kanuni moja tu ya kupenda ulimwenguni: nayo inasema hivi ‘Ili ubaki salama katika kupenda au kupendwa sharti ujipende wewe mwenyewe kwanza.’ Kama kanuni inavyosema, ukijipenda utapendeza na utapendwa. Ukipendwa pendeka nawe upende. Wasipokupenda usiwachukie. Kuwaweka watu alama eti kwa sababu hawakupendi ni vibaya sana na utaishi na moyo mpweke mpaka mwisho wa maisha yako.

Mwanangu;

Hakuna katika ulimwengu huu, aliyewahi kuishi peke yake bila watu akafanikiwa. Vilevile hakuna ulimwenguni aliyewahi kufanikiwa kimaisha akiwategemea watu. Ili ufanikiwe katika mambo yako unahitaji kukutana na watu. Japokuwa unahitaji watu unatakiwa uwe mja wa hadhari maana wakati mwingine chumvi huonekana kama sukari. Unapowatazama watu kwa macho mawili, wao wanakutazama kwa macho mengi.

Katika watu hao, wapo watakaokujaribu, wapo wengine watakutumia ili wafikie malengo yao. Na wapo wengine wataingia katika maisha yako ili wakupende na kukusaidia bila sababu. Wewe chagua watu wa kufanya nao urafiki ili msaidiane na uchague watu wengine ili mshirikiane. Ni rahisi kuwajua maana urafiki una sifa zake bainifu na moja katika sifa hizo ni kutodhuriana. Mtu mwovu hana rafiki hupata mwenza tu, mwovu mwenzie

Mtu akikugusa begani geuka upesi umtazame usoni. Ukishikwa mguu jitahidi kupunguza mwenzo na usimame kabisa. Atakayekusalimu inamisha kichwa chako kwa unyenyekevu kuitikia salamu yake. Na usisite kukunja goti lako ukikaribishwa pahala. Masikio yako usiyasimamishe kila mara kutaka kusikia kila linalozungumzwa. Wakati mwingine yatie masikio yako nta maana maneno mengine ni sumu mno na hayafai kuingia kila sikio. Na ukiufumba mdomo wako utabaki salama mbele ya kila mtu. Ukimya si dharau, ukimya ni nguvu na ujasiri kwenye nafsi juu ya mienendo na tabia za watu wengine na ngao itakayokukinga dhidi ya watu wenye kusudi la kukudhalilisha kupitia majibu yako.

Mwanangu;

Simba kwake porini si mjini. Ikiwa utamuona simba mjini ujue anafugwa. Utambuzi wa jambo hili ni mwepesi. Hakuna kitu utakachokiona kikakosa mwenyewe. Ogopa vya watu na ujitenge navyo. Hapo utaishi sana. Chambilecho wenye kauli zao, kunguru mwoga hukimbiza ubawa wake. Mjini kuna maradhi tandavu ya watu kupenda wasivyovitolea jasho. Usiwe miongoni mwao. Kuwinda vya watu iwe kazi ngumu kwako kuliko kutembea peku juu ya michongoma. Utafikwa na matatizo makubwa ukiparamia visivyokuhusu. Fanya ima fa ima upate vyako.

Ukiona kitu cha mtu kipitie mbali na uishi kwa tahadhari. Ukiwa na tahadhari utapata nguvu itakayokuwa ngao kukukinga dhidi ya majaribu ya watu. Tahadhari itakuwa kama josho la kukusafisha dhidi ya shutuma mbaya juu yako. Tia bidii upate vyako. Ukijikusuru katika kuuza ukata utanunua ukwasi. Hapo utafaulu na utaepuka kutamani vitu vya watu wengine.

Mwanangu;

Mwisho kabisa, ulimwengu una mambo mengi sana na kifo kikiwa miongoni mwake. katika mambo hayo, yapo mazuri na mabaya. Mambo mazuri hupendeza na hupendwa wakati mambo mabaya huchukiza mioyo ya wungwana. Ulimwenguni pia kuna watu wengi—wazuri na wabaya. Watu wazuri hupigiwa mfano kila mara na hufurahisha nafsi za watu wazuri pia. Bali ukiwa mtu mbaya utatengwa na walimwengu kwa siri na dhahiri. Katika ulimwengu huu pia utaviona vitu vingi mno ambavyo miongoni mwake ni vizuri na vingine vibaya. Mshahara mzuri unatokana na kuwafanyia watu vitu vizuri. Usishangae ukilipwa vibaya ikiwa hautawatendea watu vizuri.

Ilivyo, hakuna anayeyataka mambo mabaya wala anayewataka watu wabaya na vitu vibaya. Kila mmoja anayataka mambo mazuri, anataka akutane na watu wazuri na kuvitaka vitu vizuri pia. Pamoja na mambo yote hayo, mwisho wake ni nini? Mwisho wake ni kifo. Ama uwe na mambo mazuri, watu wazuri na vitu vizuri au uwe na mambo mabaya, watu wabaya na vitu vibaya katisho la yote hayo ni kifo—unakufa na unaviacha.

Kifo si kama mbwa unayemjua jina kwamba ukikitaja sana hakitakukuta. Kifo ni ahadi na ikitimia unakufa. Jambo baya ni kuwa, ukifa anayejua kuwa umekufa ni ambaye hajafa. Watu wanakufa na kuzikwa kila siku na isivyo bahati hakuna anayejiona kama amekufa wala kushuhudia mazishi yake.

Mwanangu;

Neno langu hili si chochote isipokuwa liwe waadhi na siraji kwako itie nuru kwenye giza totoro upate kuona unakokwenda. Litumie kama boya-okozi litakalokuwezesha kuelea katikati ya bahari tesi ya majojo. Ulimwengu umekuwa kama dudu liumalo ukijisahau ukalipa kidole utapata joto la firauni likuache ukiogelea kwenye machozi yako wewe mwenyewe ukiwa kwenye simanzi na moyo upate jitimai. Likuepushe na mizungu na maneno yenye kutia chonza ukazusha kitahanani. Zani si hazina ni ukuba na mwisho wake utatiwa hatiani uhukumiwe adhabu utakayoshindwa kuibeba milele. Na neno hili liwe mnunguri utakaokuponya na nyoka wenye sumu kali ya ujinga; husuda, chuki na masimango.

Basi mwanangu, hilo ndio neno lenyewe nililoona linafaa kukuusia. Wewe, kwa sababu ya umri wako, unayo nafasi kubwa ya kujifunza zaidi na ukafundisha wengine kwa ufanisi zaidi kuliko mimi.

Ndimi baba yako!