Kipenzi Shetani

Leo hii kwa akina Aisha Ramadhan kulikuwa kumefurika hadi pomoni. Shangwe, nderemo na vifijo vilisikika hewani. Ilikwa siku kuu kwa Aisha na familia yake. Watoto wa uswahilini walikuwa wana imani kuwa leo watabeba wali kwa mifuko ya khaki na mashati. Mashoga wa Bi. Mwanahija mamake Aisha walifurika si jikoni, si sebuleni, si ukumbini na hata uwanjani. Ngoma iliyokuwa pahala hapa ilikuwa ya kupasua ngoma za sogora. Viuno vilitupwa juu ndani ya madera na kanga zilizofungwa kiunoni. Wachezaji ngoma walikuwa wamejituma ni kana kwamba kucheza kule ndiko walikoumbiwa. Walipishana kwa ustadi mkubwa.

Wanasarakasi walipoingia ndani, waliwaacha wengi vinywa wazi kwa uzoefu wao wa kujenga maumbo tofauti tofauti kwa kutumia watu. Vumbi iliyokuwa hapa sitakuambia, wewe tafakari tu. Madera yaliloa jasho. Ndani ya wacheza ngoma alikuwa mwendawazimu Bw. Haji. Kichaa wa kuhuruja mengi pengine kutokana na ukichaa wake ama pengine kutokana na yaliyomghasi, lakini kwa sasa hayo yake na ukichaa wake hayatuhusu. Naam, tupo arusini ya kidosho wa kijiji cha Maweni. Binti aliyewatesa wengi kwa urembo wake.

Sikwambii ni vijana wangapi waliofika kwa Bi. Mwanahija kuleta posa zikakataliwa. Wenye pesa na magari ya kifahari walifurika lakini wapi. Ng’oo! Waliambulia patupu. “Si huyu wangu, huyu haolewi ulimwengu huu,” alisema kwa mashombo Mwanahija. Aisha alikuwa mrembo kama neno mrembo linaafiki kueleza hurulaini kama yeye. Kito cha almasi. Nywele zake za kipilipili na madera yake bulbul yalimfanya kung’aa kama mbalamwezi. Meno meupe kama theluji na midomo miekundu kama damu. Si mweupe kupitiliza, si mweusi, rangi yake hapo katikati. Mwendo wa mwanamitindo aliyebobea, kiuno cha nyingu.

Kifuani chuchu mbili zilizojaa na kusimama tisti. Macho yenye ulaghai wa kimapenzi na weusi katika kope zake. Kisha aje aongeze wanja ambao ni suna ungemwona ungelambatia. Vyote hivyo vilimkamilisha Aisha Ramadhan na ambaye anaolewa leo. Na wala usidhani mume wake kaja hivi hivi. Mlolongo wa magari yaliyokuja na mumewe na jamaa zake uliokuwa kwa akina Aisha leo hii ungefika mbinguni ungepangwa kwenda juu.

Mume huyu Aisha hakumpata virahisi kama udhanivyo. Alimpigania kutoka kwa wasichana wengine waliomtaka. Na wala vita hajavianza jana, alivianza alipokuwa mwaka wa kwanza chuo kikuu. Ni mara ngapi Aisha kampata na wasichana wengine chuoni lakini akavumilia? Ni mara ngapi Aisha amesoma arafa za mapenzi alizotumia wasichana wengine lakini akayamezea hayo? Ni mara nyingi, hazihesabiki hata kwa kikokotoo. Vita ambavyo amepigana ili kumweka mwanaume huyu vilikuwa vingi, hata leo unapomwona kapambwa eti anaolewa basi jua yeye ni shujaa.

Kungwi aliyemfunda Aisha anafaa zawadi kochokocho kwani alimpa siri ya kumuweka mwanaume vyema. Licha ya mwanaume huyu kuwa na wapenzi wengi, alimpenda na kumthamini Aisha kwa vitu viwili. Mapishi na kiuno. Vyakula alivyokuwa akimpikia walipokuwa chuoni vilimfanya mwanaume huyu kukwamilia kwa binti huyu wetu. Hapa kwa kiuno ni siri yao wawili hayo hayatuhusu. Turudi shereheni ambako kulikuwa kumewaka moto sasa.

Bi arusi alitoka nje kavaa rinda refu lililofagia chini. Kichwani kavishwa taji kama malkia. Machoni wanja na herini puani. Midomo rangi ya zambarau, mikono yote piko. Viatu kutoka urusi na maua kutoka Makkah kayashika mikononi. Upande wa mume wake Macharia ulikuwa sawa pia. Suti la thamani na viatu vya milioni kadhaa. Yote hayo yakaweka arusi hii kuwa arusi bora iliyowahi kufanyika Maweni. Wabara hawa waliona fahari kuja kuzoa mke pwani – si kuoa. Mwendawazimu Haji alikuwa akisubiri wakati wa mlo tu. Arusi ikafanywa lakini kwanza walitua kiasi. Wakauliza kama kuna yeyote ambaye angependa kupinga harusi hiyo. “Harakisheni jameni mimi nimekuja hapa kula sina mengi” haya yalikuwa maneno ya Haji.

Umati ukacheka mpaka machozi yakawatoka. “Lakini inavyoonekana hapa Mwanahija mwanao ameolewa na pesa hajaolewa na mtu. Na pesa ni shetani mama wee! hivyo sioni haya kusema binti wetu mzuri kaozwa na shetani. Harusi ya shetani hii….” Kabla ya Haji kumalizia kauli yake alibebwa akatupwa mbali. Arusi ikaendelea. Pete walivikana, busu wakabusiana na picha zikapigwa siku hiyo. Kumbukumbu zikahifadhiwa vyema kupitia picha hizo. Watu wa uswahilini wakasimama mbele ya magari ya wenyewe na kupiga picha. Ni mazoea huku kwetu.

Wakati muhimu uliwadia sasa nao ni wakati wa kukula. Vyakula vikatandikwa mezani, walaji wakajongea. Umma zikaanza kupigana na sahani. Vita vikaendelea. Wengine ni viganja na pilau, vidole na nyama, visu na samaki na wastarabu kama sisi ni glasi za sharubati mkononi, kando ndoo ya matunda anuwai.

Kuliliwa, kukaliwa na kuliwa. Vyakula vikarudiwa mpaka matumbo yakainua mikono. Mwendawazimu Haji akala mpaka akasema yatosha. “Dunia raha aisee! Siamini kuwa siku moja mimi Haji nitakufa niache vyakula vitamu kama hivi. Lakini sipendi chakula, hasaa chakula hiki cha shetani kama huyu aliyekuja kuzoa binti yetu.” Haji alisikika akisema. Sababu ya Haji kuita Macharia shetani tulikuwa hatujui wala hatukutaka kujua wakati ule. Tulichotaka kujua kwa sasa ni vyoo viko upande upi tukapunguze. “Maisha kama haya ndo natamani shoga, peana binti yako aolewe ili tuandae karamu nyingine kama hii,” alisema Mwajuma akimwambia shogake Salma.

“Kweli shoga’ngu unasema ukweli,” alijibu huku kashikilia kipande cha paja la kuku. Kwa Mwanahija siku hiyo tuliwacha vitu viwili; maelfu ya vyombo vichafu na vyoo vilivyojaa kwa sababu ya kupunguza ili tupate nafasi ya kueka vingine. Watu wakafumukana na kila mtu akaenda zake uku kabeba hiki ama kile. Vyote vyakula. Mlolongo wa magari ukachafua barabara kurudi bara. Ndani alikuwa Aisha na mumewe, wana uhuru sasa wa kufanya kile walichozoea. Hawatafika tena kwa kliniki ya Mvimbe kuzuia kuzaa mwanaharamu. Vitendo vyao vilikuwa sasa vimehalalishwa chini ya misingi ya ndoa na dini. Haoooo! Wakatokomea. Nyuma wakaacha vumbi na kumbukumbu za harusi kubwa iliyowahi kufanyika Maweni. Hadi waleo ukifika kijiji cha Maweni ulizia utaambiwa historia nzima kwa masaa kadhaa. Lakini usiulizie kichojiri baada ya arusi hiyo manake ni cha kutamausha.

*****

Mbele ya kioo alisimama kwa madaha Maimuna dadake mdogo Aisha. Ndio mwanzo kamaliza kidato cha nne na ana hamu ya kujua maisha ni nini na siri ya maisha. Na siri hii ya maisha ipo wapi ama ataijulia wapi? Mjini bila shaka. Mji nao ulikuwa ukimwita. Aisha alikuwa kajifungua kitoto cha tano sasa na alihitaji mtu wa kwenda kumsaidia katika kazi za nyumba. Lakini mbona asiandike kijakazi? Anaogopa kuibiwa bwana eti. Wewe unajua tabia za vijakazi wa mjini? Kazi ni kuiba mabwana za watu. Wito wa Maimuna kwenda kukaa kwa dadake ulikuwa habari njema kwake. Mwanahija akamsihi mwanaye ajichunge na vijana wa mjini atakapofika mjini. Akamwambia amsaidie dadake kwa kazi za nyumba na kumlea mtoto. Hayo yote Maimuna alikuwa anajua hakuhitaji kufunzwa. Mume wake Aisha akatuma nauli ya ndege kutoka pwani hadi bara mji mkuu. Maimuna akawa wa pili kupanda ndege katika kijiji kizima cha Maweni. Wa kwanza alikuwa Aisha. Alipofika mjini alipokelewa na Macharia kwa sababu Aisha alikuwa na kitoto kichanga hangeweza kufika kwenye angatuo.

Njiani, Maimuna alitazama majumba makubwa makubwa yaliyokuwa yamesheheni katika mji huu. Wakati huu wote Macharia alikuwa akimtazama kupitia kioo cha gari. Alipenda alichoona. Maimuna alikuwa mweupe pepepe! Na mrembo kupindukia. Moyo wa Macharia ulipiga kwa kasi. Alikuwa kavutika na binti huyu. Mapenzi hayana macho eti. Aligutushwa na honi iliyopigwa kuashiria wafunguliwe lango kuu. Mandhari ya nyumba ya Aisha yalipendeza. Ukuta wa mawe ulizunguka jumba hilo, juu yake nyaya za umeme kuzuia wezi. La, kutisha wezi. Mwizi hazuiliki. Uwanja mdogo uliokuwa na nyasi zilizokatwa vizuri. Maegesho ya magari ambapo palikuwa na magari yasiyopungua sita. Mbele ya nyumba kidimbwi cha kuogelea. Jumba lenyewe lilikuwa la rangi ya dhahabu.

Waliingia ndani, ilimchukua Maimuna siku mbili kugundua kuwa mle langoni mlikuwa na kengele. Aisha na dadake walipigana pambaja na kufurahi kuonana. Walipiga soga nyingi huku Aisha akiulizia habari za nyumbani. Wana wa Aisha wanne walikuwa shuleni Maimuna alipofika. Miaka kumi na tano ndoani si mchezo. Mwana wa kwanza wa Aisha alikuwa Zuhura naye alikuwa kidato cha pili sasa shule ya bweni yenye jina lisilotamkika. Wa pili alikuwa mvulana, darasa la nane naye pia shule ya bweni. Watatu na wanne walikuwa mapacha. Wote darasa la nne nao vile vile shule ya bweni. Alafu hapa nyumbani kulikuwa na kitoto kichanga ambacho kilichukua sura geni. Jambo hili lilimtia wahaka Macharia akaagiza msimbo-jeni ufanywe. Matokeo yakamridhisha ila ile sura bado akatilia dukuduku.

Miaka kumi na tano ya ndoa baina ya Aisha na Macharia haikuwa rahisi. Ni mara ngapi Macharia amelala nje? Ni mara ngapi karudi ananuka marashi ya mwanamke? Tabia ni ngozi. Alikuwa mkware. Yakini Macharia alikuwa si mume. Alikuwa na wanawake wengi na ambao hata yeye mwenyewe alikuwa hakumbuki. Fununu zilisema alikuwa na jumla ya watoto ishirini ambao walijulikana. Nakupa kazi tafakari ni wangapi hawakujulikana. Wanawake alibadilisha kama viatu. Mikahawa ya kifahari ndiko kulikokuwa kichinjio chake. Hakuna mhudumu wa kupeana vyumba katika hoteli zote mjini ambaye hakumjua.

Alipendwa na wanawake, alikuwa kama ua na wanawake wake walikuwa kama nyuki. Walihitaji nta, na nta raha kupata hasa harufu yake yakupendeza. Lakini nta ghali kupata pia hasa kama ilitoka kwa bwana Macharia. Ina malipo na malipo yake si ghali, muradi uwe tayari kuuza mwili wako ili kupata nta hii. Ungeridhia? Ni muhali kukataa kwani asali nayo ni tamu zaidi kuliko nta ila nta ni malighafi ya kutengeneza asali hii. Almuradi hakuna kizuri kipatikanacho virahisi.

Vita katika ndoa yao ilikuwa ni lazima. “Utakuja kuniletea gonjwa humu ndani mume wangu,” alisema Aisha usiku mmoja huku akisinasina kwa kilio. Alijibiwa kwa kofi moja lilomtuma hadi sakafuni. Akabusu sakafu. Walipigana, wakapigana hadi wakachoka. Mume mwenyewe naye kifyefye hana nguvu. Nguvu zake kuna kule ambako huenda. Hiyo ni siri yake mimi sijui ama wewe unajua?.

Aisha na Maimuna walikuwa na mlahaka mwema. Waliishi vyema mle ndani huku wakisaidiana kukilea kitoto kile kichanga. Maimuna alinunuliwa simu na kuanza kuzama katika mitandao. Alitaka kujua siri ya maisha na alikuwa kaambiwa kuwa siri ya maisha ukitaka kuijua nenda mjini. Sasa yupo mjini. Alisakura waliozaliwa mjini katika mitandao ili wamfunze siri ya maisha. Waama mitandao imefanya dunia kuwa kama kijiji kidogo. Alijifunza mengi mitandaoni mazuri na mabaya. Mwisho akajumuisha masomo yake pamoja na kuyahakiki tena na tena akagundua kuwa kuna siri moja ya maisha duniani. Pesa.

Katika utafiti wake aligundua kuwa pesa hazipatikani sana sana kwa vijana. Zinapatikana kwa wazee. Alihisi vibaya pale alipogundua kuwa wazee hawa wenye pesa wengi wao kama si wote wameoa. Hii ni kusema kwamba lazima awe na mume wa mtu ili kupata pesa, na pesa hizi ni za nini? Mapambo bila shaka. Mwanamke ni mapambo. Aliwaza na kuwazua pa kutoa mtu mwenye pesa ambaye atakuwa anamkimu akakosa. Sababu za kukosa zilikuwa dhahiri. Kwanza alikuwa hajui jiji vizuri na pili alikuwa haruhusiwi kutoka nje.

Ndipo alipomjia shetani na kumuambia “ya nini uandikie mate na wino upo?”. Akajidadisi akaona anatosha. Naam anatosha kucheza vyema kama si kuchezesha. Anatosha kuhesabu nyota vyema tena kwa masaa mengi. Anatosha kustahamili. Sasa ilibaki jambo moja tu. Mbinu za windo lake. Alijua vyema kuwa windo hili lake lilikuwa haramu kuwinda kwa sababu lilikuwa miliki ya mtu. Na si mtu tu bali mtu aliyekuwa nasaba yake. Kwake windo wala kitendo hakikuwa haramu. Aliamini hamna haramu mjini. Mikakati akaipanga ikapangika.

Alianza na kuvaa nguo fupi fupi kila muda alipokuwa nyumbani.

“Dada’ngu jamani jisitiri, mwanamke ni stara,” alimwambia Aisha.

“Lakini dada si tupo wawili hapa kwa nyumba tena mimi huwa sitoki nje daima,” angejibu kwa kusonya.

“Vipi akikupata mume wangu hivyo ulivyo,” alizidi kusaili Aisha.

“Yeye huja jioni tena usiku wa manane atanionaje? Nitakuwa nimelala,” alijitete vya kutosha.

Uwepo wa Aisha kila saa pale nyumbani ulichelewesha mengi. Ilitakiwa hata apeleke mwana kliniki peke yake siku moja ndipo yaliyopangwa yatimie. Macharia akawa anatumiana arafa na Maimuna kila siku. Mapenzi yakakolea. Akamwahidi mengi. Naye Maimuna alikuwa amuahidi jambo moja tu. Wewe unaona ni lipi? Walichoahidiana ni siri yao tuwachie wao.

*****

Siku moja Macharia alirudi nyumbani mapema. Ilikuwa saa mbili hivi. Siku hii alionekana mchangamfu sana tena mwenye bashasha si haba. Chakula kikatandikwa mezani wakala. Aisha alikuwa anawangwa na kichwa siku hiyo na jino pia. Hakuwa mwingi wa maneno. Soga kati ya Macharia na Maimuna zilikolea.

“Unataka kuwa nini pindi matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yatakapotangazwa?” alimuuliza Macharia alipokuwa akikata kipande cha nyama kwa kisu.

“Napania kuwa mwanahabari,” alijibu kwa bashasha.

“Kweli unaweza kuwa, una sura na umbo la uanahabari. Hasaa mtangazaji wa runinga, utawanasa wengi,” alisema huku akicheka.

Ni ajabu kugundua hadi waleo watu bado udhani kuwa mtangazaji bora ni umbo na sura. Aisha aliomba kwenda kulala manake alikuwa ahisi vyema. Akachukua barafu kwenye jokofu na kuingia chumbani. Akafunga mlango.

Macharia alijongea alipokuwa Maimuna. Kisadfa umeme ukapotea kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha usiku huo. Kawaida ya Afrika umeme kupotea kunaponyesha sana. Tumezoea. Wapenzi hawa wa siri waliketi sako kwa bako wanatazamana kwa macho yenye uchu. Mkono wa Macharia ulizuru katika mapaja ya Maimuna na kuanza kumgusagusa kwa kumpapasa. Maimuna akalegea.

Alimbeba juu kama mtoto mchanga. Huyooo! Hadi chumbani mwa Maimuna wakaingia na kufunga mlango kwa kishindo kikubwa. Walichofanya humo ndani hata nami natamani nijue. Waligutushwa mlango ulipofunguliwa ghafla tena kisadfa umeme ukarejea. Kitandani walilala watu wawili kama walivyozaliwa wote. Kando yao alisimama Aisha na ambaye alikuwa kaamshwa na jino lililomuuma. Alipomkosa mumewe akaamua akwende kwa dadake Maimuna kumuulizia aliko. Alichokipata kilimkwatua moyo. Wachezaji wawili walimiliki mimbari hii. Wote wameloa jasho mwili mzima. Ishara ya kuwa hawakuwa wametoka kufanya dogo. Usukuti ulitawala chumba. Wahusika wote wawili wamemwangalia mtazamaji wao. Ni kana kwamba wanamwambia “tumechoka kuigiza, mchezo umeisha. Njoo kesho”.

Aisha alisinasina kwa kilio “Nilijua ujio wako mjini ni uchuro” akatoka ghafla na kufululiza hadi chumbani mwake. Kesho yake asubuhi alimpigia mamake simu na kumweleza kila kitu.

“Uliniletea mke mwenza mjini mama,” ndivyo alivyoanza.

“Uliyataka mwenyewe mwana’ngu nilikuambia utafute kijakazi ukakataa. Kesho jioni nitakuwa huko mjini mnieleze kilichotukia”. Hiyo ndiyo iliyokuwa kauli ya mwisho ya Mwanahija.

*****

Machweo ya siku iliyofwata yalimpata kwa Aisha nyumbani. Aliketi wa wanawe wawili ukumbini. “Ulikuja kumsaidia dadako ama ulikuja kuwa mke wa pili wa mume wake?” alikuja juu kama moto wa kifuu Bi. Mwanahija. “Naapa sitarudia mama” alinyenyekea Maimuna. Aisha alikuwa akilia tu. Mwanahija alimzomea mwanawe hadi pale Macharia alipofika.

Baada ya kula chajio Mwanahija alitaka kuzungumza na Macharia. Macharia naye akakataa katakata kuzungumzia lolote pale ndani nyumbani. Akamtaka mama mkwe wakwende aghalabu hotelini ndipo waseme zaidi. Aisha akaridhia kwa sababu alitaka suluhu. Wakaondoka na kuahidi kurudi baada ya nusu saa. Macharia alimpeleka mama mkwe katika mkahawa wa Nyota uliokuwa mjini katikati. Wakaketi katika meza moja na kuagiza soda. Mwanahija akawa anamuuliza Macharia mbona akafanya ubatara ule. Walizungumza, wakazungumza na kuzungumza mengi tunayojua na tusiyoyajua.

Nusu saa iligeuka ikawa saa. Walirudi nyumbani kesho asubuhi. Walionekana kupata suluhu. “Kwanza naomba msamaha kwa kutorudi usiku wa jana. Tulimaliza mazungumzo saa sita usiku na hivyo tukaona ni bora kulala hotelini. Nikamlipia mama chumba akalala huko,” alisema Macharia. Aisha hakuwa na wasiwasi na hilo, alijua vyema kuwa huyu alikuwa mamake mzazi na mamake mzazi hangekubali kufanya maovu na mume wa mwanawe. “Suluhu ni hii, nitarudi na Maimuna kijijini nadhani mtoto sasa ashakuwa unaweza kumlea. Nawe utabaki na mumeo hapa mjini ameahadi kuwa atabadilika,” alisema Mwanahija. Baada ya kuzumgumza Bi. Mwanahija na Maimuna waliondoka kurudi kijijini huku Aisha akibaki na mume wake.

*****

Baada ya miezi miwili, Aisha alionekana nyumbani kabeba mwanawe mgongoni na kando yake kifungua mimba Zuhura. Leo hii alikuwa kaletwa na jipya. Alipofika alimkuta mamake kaketi mkekani anakuna nazi. Nyumbani alikuwa mwendawazimu Haji ambaye alikuwa kaomba kazi kulima shamba na akapewa. Ilikuwa adhuhuri, wote walikuwa wanakula chamcha. Aisha alimwendea mamake na kumwangukia miguuni huku akilia. Zuhura alikuwa kasimama huku kajishika kiuno. Alikuwa mjamzito.

“Mama mimi sikuolewa na mume niliolewa na ibilisi,” ndivyo alivyoaanza Aisha.

“Niliwaambia siku ya ndoa kuwa mumeo ni shetani hukunisikia,” haya yalikuwa maneno ya mwendawazimu Haji.

“Amefanya nini mumeo mara hii mwanangu?” Aliuliza Mwanahija.

“Amemtia mimba mwanawe huyu hapa Zuhura”.

“Tobaaaaa! Mungu wangu, huyo ni mtu ama ni ibilisi jamani?” Aliuliza Haji huku akiruka juu.

“Si mkubwa hayo sisi tunayo makubwa tuliyokuandalia humu,” alisema Maimuna.

“Yepi hayo? nielezeni mama,” alitaka kujua Aisha.

“Sasa hivi unavyoniona nina ujauzito wa mume wako…” alianza Maimuna. “Siku ile uliyonifumania na mume wako hiyo ndiyo siku aliyonitia mimba mumeo. Huyo unayemuona hapo akaketi ana mimba ya miezi miwili hiyo nayo akaipata siku ile walipoenda hotelini kuzungumza kuhusu hatua ya kuchukua juu yangu na mumeo”. Aisha hakuamini masikio yake. Alianguka akazirai.

“Yaani familia nzima hii mna mimba ya mtu mmoja?” mwendawazimu Haji aliuliza ila hakupata jibu. Wote wawili walikuwa wakisinasina kwa vilio. Mwanahija hakuamini haya.

“Nitaficha wapi sura yangu jamani?” Alijiuliza asipate jibu.

Baada ya kukaa pale wiki tatu, Aisha alimwacha mwanawe mjamzito na kurudi mjini tena kwa mumewe. Alikutana asubuhi ile na Haji. “Mbona unarudia tena mkono uliokukata? Huoni kuwa mumeo si mtu jamani ni shetani huyo. Umewaacha nyuma watu watatu walio na mimba yake. Hauoni aibu jamani?” Haji alimuuliza huku kaghadhabika. Jibu la Aisha lilimwacha Haji kinywa wazi siku hiyo. “Nampenda alivyo. Ndiye kipenzi changu. Naam, ndiye kipenzi shetani”. Baada ya siku kadhaa taarifa zilimfikia Aisha mjini kuwa mamake na dadake walikuwa wamejitoa uhai. Wangestahamili aje aibu ile? Ingekuwa wewe ni Maimuna au Mwanahija ungefanya nini?

Maswali 1. Jadili ufaafu wa anwani Kipenzi Shetani (Alama 20)

2. Mwendazimu Haji ni mwendazimu timamu. Thibitisha kauli hii. (Alama 20)

3. “Kweli shoga’ngu unasema ukweli” Eleza muktadha wa dondoo hili (Alama 4)

Jadili madhara ya ukweli unaosemwa na msemaji wa dondoo hili (Alama 16)

KIPENZI SHETANI

Alisema kwa mashombo – alisema kwa maringo.

Hurulaini – mwanamke mrembo kupindukia.

Kungwi – mtu ambaye hufundisha mwari mambo ya jando.

Mlahaka – hali ya kupatana na kuingiliana na watu vizuri.

Kuhujuru – kuporoja au kusema mengi.

Bulbul – nzuri au -enye kupendeza.

Mimbari – jukwaa.

Usukuti – kimya.

Uchuro – enye kuleta matatizo.

Ubatara – mambo maovu.

Angatuo – uwanja wa kutua ndege.